Prof. Ntalikwa: Gesi Mtwara Ipo kwa Wawekezaji

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prof. Justin Ntalikwa amesema kuwa kiwango cha gesi asili kilichopo Mtwara kinauwezo wa kutumika kwa viwanda vipya vya mbolea Mkoani Mtwara.

Prof. Ntalikwa amesema hayo mwishoni mwa juma katika ziara yake Mkoani Mtwara ya kujionea maeneo ya uzalishaji na utafiti wa gesi asilia Mkoani humo.

“tumejiridhisha kwamba kiasi cha gesi kitakachopatikana kinatosha kabisa kwa ajili ya kiwanda cha mbolea kinacho tarajiwa kujengwa Mkoani Mtwara,” alisema Prof. Ntalikwa.

Alisema kuwa katika eneo la Ntorya, Halimashauri ya Mtwara ambako Kampuni ya Ndovu Resources inaendesha utafiti wa gesi asilia tayari kumekwisha gundulika gesi na kinachofanyika sasa ni uhakiki wa hifadhi ya gesi hiyo.

“Kisima cha kwanza cha gesi kimekwisha gundulika kiasi cha gesi cha futi za ujazo trilioni 0.15,” alisema Prof. Ntalikwa.

Alifafanua kuwa, kisima cha pili kinatarajiwa kuchimbwa na kinakadiriwa kuwa na futi za ujazo trilioni 0.9, huku kisima cha tatu kikitarajiwa kuwa na futi za ujazo 1.5.

Alisema eneo jingine lilionekana kuwa na uwezekano wa kuzalisha gesi asilia ni eneo la Msimbati liliko Halimashauri ya Wilaya Mtwara.

“Kampuni ya Maurel and Prom (M & P) pia wameonyesha wako tayari watakapo hitajika kuchimba visima vingine kwa ajili ya uzalishaji kufanya hivyo,” aliongezea Prof. Ntalikwa.

Prof. Ntalikwa alisema kuwa kunatarajiwa kujengwa Kiwanda cha Mbolea cha Kampuni ya Helm ya Ujerumani Mkoani humo huku kihitaji kiasi cha gesi cha futi za ujazo 0.8 kwa kipindi cha miaka ishirini.

Alisisitiza kuwa maeneo hayo yote yanauwezo kwa kutoa gesi ya kutosha kwa ajili ya Kiwanda hicho cha mbolea na kwa kampuni nyingine zitakazo wekeza Mkoani humo.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bi. Halima Ndendegu alishukuru kwa ziara ya Katibu Mkuu Mkoani Kwake kwa kuhakikisha upatikanaji wa gesi asilia kwa wawekezaji.

“Nimefarijika sana kwa hii ziara ya leo kwani katika ziara nzima mmeweza kuona wawekezaji walivyotayari kupokea miradi,” alisema Bi. Dendegu.

Aliongeza kuwa uhakika wa upatikanaji wa gesi ni hatua moja mbele katika kuhakikisha uwekezaji katika sekta ya viwanda unatokea Mkoani Mtwara.

“nimeridhishwa na zile taarifa za kitaalam ambazo nimezipata, lakini kubwa zaidi pale nilipoambiwa hata nikitaka gesi leo kama niko tayari na mwekezaji naweza nikapata,” asisitiza Bi. Dendegu.

Kwa upande waka, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapuulya Musomba alisema kuwa TPDC inakazi kubwa ya kuhakikisha gesi inapatikana kwa ajili ya viwanda nchini.

“Kitendo cha watu kuwepo wanahitaji gesi kwetu sisi ni faraja kubwa na ndio kazi kubwa tunatakiwa tuifanye,” alisema Mahandisi Musomba.

Ameleza kuwa TPDC iko tayari kuona inashirikiana na wawekezaji ili kukidhi mahitaji ya viwanda ambavyo vinatarajiwa kujengwa Mkoani Mtwara.

“Ujio wetu hapa Mtwara ni kuhakikisha viwanda vitakavyojengwa Mtwara vya mbolea na kemikali vinapata gesi asilia,” aliongeza Mahandisi Musomba.

Kampuni ya Helm ya Ujerumani inatarajia kujenga kiwanda cha mbolea katika eneo la Msanga Mkuu lenye ukubwa wa hekta mianne (400), Mkoani Mtwara.


Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *